Kongamano hilo litawakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na wenzao kutoka mataifa ya Kiarabu ili kujenga ushirikiano na kutafuta masoko mapya.
Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) limewaalika wafanyabiashara kutoka sekta mbalimbali nchini kushiriki kongamano la biashara litakalofanyika Dubai. Kongamano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano na Consumer Choice Awards Africa na TanTrade.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Deogratius Massawe, amesema wafanyabiashara watapata nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na wenzao kutoka mataifa ya Kiarabu kupitia mikutano ya kibiashara (B2B). Hapo wataweza kutafuta washirika, kujadili fursa za uwekezaji na kujifunza jinsi ya kuingiza bidhaa na huduma zao katika masoko mapya.
Washiriki pia watakutana na taasisi za serikali na kupata maelezo kuhusu huduma na msaada unaopatikana kwa ajili ya kukuza biashara zao.
Massawe amesisitiza kuwa wafanyabiashara ambao hawakuteuliwa kuwania tuzo za Consumer Choice Awards pia wanakaribishwa. Wanaweza kutumia kongamano hilo kutambulisha bidhaa na huduma zao kwa wafanyabiashara kutoka nje ya nchi.
